NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, ametoa rai kwa vikundi vya maendeleo vilivyonufaika na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kuitumia mikopo hiyo kwa matumizi sahihi sambamba na kukumbuka kuirudisha ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kupata nafasi ya kukopa.
Mhe. Mgomi ameyasema hayo mapema leo Novemba 20, 2024 wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya asilimia Kumi kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Community Center uliopo wilayani Ileje.
DC Mgomi amevipongeza vikundi vya maendeleo vilivyopata mkopo huo sambamba na kuvihimiza kuwekeza katika shughuli walizojipangia ili kupata faida pamoja na kurudisha marejesho ya mkopo huo.
Mhe. Mgomi pia amemshukuru Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali masilahi ya wananchi wa Wilaya ya Ileje kupitia mikopo hiyo inayolenga kuimarisha hali ya kiuchumi ya vikundi vya maendeleo.
Katika hatua nyingine DC Mgomi amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba kwa kusimamia na kuhakikisha zoezi la utoaji wa mikopo linakwenda vizuri.
Mwisho.