Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa wilaya ya Ileje Bi Farida Mgomi, amewaasa watanzania kuendelea kudumisha umoja, amani, upendo na mshikamano akiamini kwa kufanya hivyo ni kuimarisha Tunu ya msingi wa maendeleo katika Taifa lililoasisiwa na hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume.
Bi Mgomi ameyasema hayo mapema leo katika Kongamano la Maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika lililofanyika katika ukumbi wa Community Centre Wilayani Ileje.
DC Mgomi pia amewahimiza wananchi kuendelea kuzienzi Tunu zilioachwa na waasisi wa Taifa ambapo kupitia Upendo Amani Umoja na ushirikiano Taifa litazidi kusonga mbele katika nyanja zote za maendeleo na kuwa mfano bora kwa Mataifa mengine.
Katika hatua nyingine Bi Mgomi ametoa pongezi kwa watumishi katika Wilaya hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha Wilaya ya Ileje inasonga mbele katika kufanya maendeleo.
Aidha amewasisitiza watumishi wa umma kuendelea kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa kwa kila mtu ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa wananchi bila kujali itikadi zao ikiwemo dini, kabila au rangi.
DC Mgomi amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya Ileje kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania ili amani na mshikamano viendelee kudumu.
Mwisho.