MMWAKAGENDA MBUNGE WA VITI MAALUM NA SIASA ZA UKOMBOZI KWA WANAWAKE
Mbeya

Na Hellen Nachilongo 

MOJA ya sababu ambazo zimechangia nchi yetu kutopata maendeleo makubwa kulingana na rasilimali ilizonazo, ni kukosekana kwa viongozi wengi wenye utashi wa kweli wa kutumikia wananchi.

Viongozi wengi hasa wanaume wamekuwa wakijali maslahi yao binafsi ikilinganishwa na wanawake. Wanaume wameendelea kutumia mfumo dume kushika nafasi nyingi za uongozi matokeo yake wanawake wenye uwezo wamejikuta wakiachwa nyuma.

Hata hivyo wanawake ambao wamedhubutu na kupata nafasi za uongozi wameonesha wazi kwamba wanaweza kuwaletea maendeleo Watanzania kama ambavyo tunaona kasi anayoenda nayo Rais Samia Suluhu Hassan.

Nyuma ya Rais Samia wapo wanawake wengi ambao wameonesha uwezo mkubwa wa kutumikia jamii, ikiwa ni pamoja na kutetea haki za watoto na wanawake.

Mmoja wa wanawake hao ni Sophia Mwakagenda (54) ambaye anasema wazi kwa kinywa chake kwamba; ” Nitaendelea kuwahamasisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, kuwawezesha vijana na kutetea haki za wasichana na watoto. Nitakuwa karibu na jamii kwa kadri nitakavyoishi.”

Mwakagenda ni mwanasiasa na mbunge kupitia Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) na amekuwa mfano wa kuigwa kwenye masuala ya uongozi.

Mwakagenda ambaye ni mbunge wa viti maalum, mwakilishi wa wanawake na amekuwa akihudumu kwenye nafasi hiyo tangu mwaka 2015 hadi sasa. Mbali na nafasi yake ya kisiasa, anafahamika sana kama mtetezi wa haki za wanawake, mchambuzi wa masuala ya kijinsia kwa zaidi ya miaka 20, na mshindi wa tuzo za kimataifa kwa mchango wake mkubwa katika kutetea haki za wanawake.

Licha ya mafanikio yake na nafasi yake ya uongozi, Mwakagenda anaamini sana katika uwezo wa wanawake na amefanikiwa kuwawezesha wanawake na wasichana zaidi ya 500 kupata mafunzo ya ushonaji na kuwapatia mashine za kushonea.

Zaidi ya hayo, aliingilia kati kuokoa ndoa za mabinti wawili waliotarajiwa kuozeshwa ili familia zao zipate ng’ombe 75 kama mahari.

Kujitolea kwa Mwakagenda katika masuala ya kijinsia, ushiriki wa kijamii na masuala ya kisiasa ni jambo lililokita mizizi ndani yake,ni hamasa ya kiasili ya kutetea haki za wanawake na wasichana katika kila kona ya nchi yake.

Alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum, hatua yake ya kwanza ilikuwa kurejea kijijini kwao Mbeya, ili awe karibu na jamii yake, kuwajua zaidi, na kushiriki katika kutatua changamoto zao.

Katika nyakati za huzuni au furaha, alikuwa mstari wa mbele kusimama na watu wake. Ikiwa kuna msiba katika jamii, alikaa na familia husika, kuomboleza nao na kuwafariji mpaka mwisho wa msiba.

Vilevile, katika nyakati za sherehe, alijiunga na jamii kusherehekea mafanikio pamoja nao.

Licha ya kujituma kwake, si kila mtu alielewa chaguo lake. Wabunge wenzake walikuwa wakimdhihaki, wakijiuliza kwa nini alichagua kubaki kijijini licha ya nafasi yake kubwa ya uongozi.

“Wabunge wenzangu walikuwa wakinicheka, wakisema ningekufa maskini nikiendelea na kijiji na kuzingatia sana jamii. Lakini hilo halijawahi kuwa kikwazo kwangu,” anasema.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, kuwa na mume mwenye msaada kumemfanya kuwa alivyo leo. Mwakagenda anaamini kuwa wanawake na wasichana wanaweza kufanya lolote sawa na wanaume, anaongeza kuwa harakati za jinsia zimewezesha maendeleo ya kijamii.

***Hadithi za watu aliowagusa maishani

Katika jitihada za kutambua mchango wake, mwandishi wa habari alizungumza na watu mbalimbali katika maeneo kama Mbeya, Chalinze, Geita na Lindi ili kujua uzoefu wao na jinsi alivyogusa maisha ya watu.

Mkazi wa Chalinze, Mbapai Mbokoso, anasema kupitia Mwakagenda, binti yake hakuolewa katika umri mdogo.

“Kama unavyojua, sisi Wamasai tunapendelea binti zetu kuolewa mapema ili tupate ng’ombe kama mahari. Lakini kupitia yeye, binti yangu Happy Mbosoko, ameweza kumaliza shule ya sekondari,” alisema Mbokoso.

Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Tukuyu, Amina Makamba, anamsifu mbunge kwa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike shuleni. “Wakati wanafunzi wa kike wanapokuwa kwenye hedhi zao, wanakosa masomo kwa sababu wengi hawawezi kununua taulo za kike.

Tunashukuru kwa kuwa Mwakagenda ameendelea kusaidia wanafunzi wa kike na kuwapatia taulo za kike,” anasema mwalimu mkuu.

Mwenyekiti wa Chama Cha Ushikrika, Rungwe Organic Tea, Magdalena Mwasandale alisisitiza jinsi Mwakagenda alivyojitolea kwa wakulima na kuhakikisha bei ya chai inapanda hadi sh.366 kutoka sh. 320 kwa kilo.

Mwasandale naongeza kuwa, Mwakagenda pia amewezesha uhamasishaji kwa wanawake wa Rungwe juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, na hivyo kuwaondolea mzigo wa kukusanya kuni na kuwaruhusu wanawake kufanya shughuli za maendeleo.

Mbali na hayo, Mwakagenda kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini wanawake ametoa msaada mbalimbali, ikiwemo nepi, sukari, sabuni, na juisi kwa akina mama waliyojifungua na waliokuwa wakisubiri kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, alimpongeza mbunge kwa kukubali ombi lake la kushirikiana na wachimbaji wadogo wanawake kutoa bidhaa mbalimbali kwa akina mama. Mkuu wa Mkoa huyo alisema,

“Tunamshukuru mbunge wetu Mwakagenda na wachimbaji wadogo wa kike kwa msaada wao kwa akina mama katika hospitali yetu ya Geita.”

***Tuzo na Heshima kwa Mchango Wake

Mwakagenda amepokea tuzo mbalimbali kwa kazi yake ya kuendeleza haki za wanawake na watoto. Moja ya tuzo maarufu ni ile ya ‘Women of the Decade in Public Life’ aliyopokea katika Jukwaa la Kiuchumi la Wanawake (WEF) huko New Delhi mwaka 2018.

Alipewa heshima hiyo kwa mchango wake katika elimu, afya, na uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake na watoto nchini Tanzania.

Pia aliheshimiwa na Taasisi ya Coady International Institute/CIDA nchini Canada mwaka 2012-2013 kwa mchango wake katika kuunga mkono usawa wa kijinsia na haki za kijamii Tanzania.

Tuzo hizi ni ushuhuda wa nafasi yake hai katika kusaidia usawa wa kijinsia na haki za kijamii nchini.

Kwa kuongeza, Mwakagenda ameanzisha mikutano na madiwani, watendaji wa kata, na wananchi kwa lengo la kuwahamasisha juu ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu wilayani Rungwe.

Kupitia mpango huu, aligawa majiko ya gesi kwa watendaji wa kata na wananchi kama hatua muhimu ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Kama mbunge, ametimiza jumla ya michango 76, ameuliza maswali ya msingi 30, maswali ya nyongeza 139, na kumuuliza Waziri Mkuu maswali matano.