WANUFAIKA TASAF WAPEWA ELIMU MATUMIZI YA FEDHA.
Songwe

By Naomi Achieng'

Songwe.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mheshimiwa Farida Mgomi, amewahimiza wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya Masikini (TASAF) katika Kata ya Mlale wilayani Ileje mkoani Songwe, kuzitumia vizuri fedha wanaozipata kupitia mradi huo kwa kuwekeza katika shughuli za maendeleo ili kuweza kujinusuru katika wimbi la umasikini.

Akizungumza katika Kijiji cha Yuli kilichopo katika kata ya Mlale wilayani hapa, Mhe.Mgomi amewasisistiza wanufaika wa mradi huo kuzitumia fedha za TASAF kwa matumizi yaliyokusudiwa na Serikali ili pale watakapohitimu katika mpango huo,wawe wamenufaika na pia kutimiza adhima ya Mpango huo wa Serikali kwa kujiondoa katika wimbi la umasikini.

Aidha, Mhe. Mgomi amewaaagiza  makatibu  Kata, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Ugani na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuweka mpango maalum wa wanufaika kuvitunza, kuimarisha na kuviendeleza vikundi vyao ili kujikimu kimaisha na kuendeleza shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kunufaika na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yetu.

Katika hatua nyingine Mhe. Mgomi amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali na kuziinua kaya Masikini kupitia Mpango wa TASAF ambao mpaka sasa kaya mbalimbali katika Wilaya ya Ileje zimenufaika.

Mwisho.