By Naomi Achieng'
WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AWAJULIA HALI MAJERUHI 40 MUHIMBILI, 35 WARUHUSIWA KWENDA NYUMBANI.
Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muunganowa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim amewatembelea majeruhi 40 wa ajali ya ghorofa lililoporomoka huko Kariakoo ambao wamepokelewa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kufanyiwa uchunguzi na matibabu.
Mhe. Majaliwa amewataka ndugu jamaa na marafiki ambao ndugu zao wameguswa na ajali hiyo kuendelea kuwa watulivu wakati watoa huduma wakiendelea kuwahudumia ndugu zao huku vikosi vya uokozi vikiendelea na jitihada za kutafuta watu wengine ambao bado hawajaokolewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi amemueleza Mhe. Majaliwa kuwa baada ya kupokea majeruhi hao, watoa huduma waliwafanyiwa vipimo stahiki na kubaini kuwa walipata majeraha sehemu mbalimbali za mwili, kisha kupata matibabu na hadi kufikia saa 11 jioni ya leo majeruhi 35 kati yao 40 wameruhusiwa kwenda nyumbani na watano kati yao bado wanaendelea na matibabu ambapo wanne wamepelekwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya matibabu zaidi.