Na Mwandishi wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Wakazi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ili wawe na sifa ya kutimiza haki yao kikatiba ya kuwachagua viongozi katika maeneo wanapoishi.
Rais Samia ametoa wito huo leo Oktoba 11,2024 mara baada ya kushiriki katika zoezi rasmi la uandikishwaji kwenye daftari hilo lililofanyika katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Chamwino Ikulu, Kitongoji cha Sokoine.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika kituo hicho, Rais Samia amewapongeza kwa kujitokeza kwa wingi, pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kushiriki zoezi hilo la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa amani na utulivu.
"Kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (Public Holidays Act) Sura 35, nilitangaza kuwa Novemba 27, 2024 kuwa siku ya mapumziko ili kuwaruhusu wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,"amesema.
Uandikishaji wa wakazi uneanza leo na utamalizika Oktoba 20,mwaka huu.
Viongozi wanaochaguliwa ni wenyeviti wa vijiji,vitongoji,mitaa na wajumbe wa mamlaka hizo.