WANANCHI SONGWE WAIPOKEA KAMPENI YA SAMIA LEGAL AID
SONGWE

Na Mwandishi Wetu, Songwe

MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amepongeza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama ya Samia (Samia Legal Aid) kwani katika mikoa ambayo imefikiwa na kampeni hiyo imeonesha umuhimu wa pekee wa kuongeza wigo wa ufikiaji haki kwa wananchi hususan walio pembezoni na ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili.

Mhe. Mgomi amesema kampeni hiyo imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria, jambo ambalo ni muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini.

Amesema kupitia kampeni hiyo migogoro mingi ya kifamilia na kijamii  iliyodumu kwa muda mrefu imesuluhishwa, ambapo hali hiyo imeleta utengamano katika familia, tija katika jamii  hususan kuongeza kipato katika uzalishaji kwa kupunguza muda mwingi kutumika katika kutatua migogoro mahakamani.

"Niwasihi wananchi wa Songwe kuitumia vema fursa hii ambayo nasi tumebahatika kuipata," amesema DC Mgomi.

DC. Mgomi ametumia fursa hiyo kushukuru uogozi wa Wizara ya Sheria na Katiba kwa namna ambavyo unaratibu na kutekeleza kampeni hiyo.  

"Napongeza timu yangu ya mkoa wa Songwe kwa namna ambavyo mmepokea  na kutambua umuhimu wa kampeni hii na ni dhahiri mmesimamia ipasavyo  maandali ya utekelezaji wa jukumu hili hapa mkoani kwetu," amesema DC. Mgomi kwa niaba ya RC Chongolo.

Aidha ameongeza kuwa Wizara ya Sheria na Katiba imepewa dhamana ya kutekeleza majukumu ya Serikali yanayohusu  masuala ya Katiba na Sheria za nchi, ambazo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha  nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya haki na utawala bora.

"Katika utekelezaji wa majukumu haya wizara imeendelea kuzingatia miongozo  mbalimbali ya kisera, kisheria, kikanuni na taratibu mbalimbali pamoja na maazimio ya kikanda na kimataifa ambayo nchi yetu  imeridhia katika kusimamia  masuala ya haki na utawala bora,"amesisitiza na kuongeza;

"Majukumu hayo yanatetekelezwa kwa kuzingatia dhima ya Wizara  ya Sheria na Katiba ambayo ni kuwa na mfumo madhubuti ya sheria na kikatiba katika kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa letu."

Aliongeza kwamba dhima hiyo inahimiza ubunifu wa mazingira wezeshi ya upatikanaji haki na huduma bora za kisheria kwa wananchi.

"Hivyo ni matarajio ya Rais Samia na Watanzania kwa ujumla  kuona Wizara hii inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi  na kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za kisheria kwa wakati na bila upendeleo wa aina yoyote," amesema DC Mgomi.

Amefafanua kwamba Wizara ya Sheria na Katiba imejipanga kikamilifu  kuhakikisha kuwa wananchi, Watanzania wananufaika na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

"Sabamba hilo katika kuhakikisha nchi yetu inaongozwa kwa  kufuata misingi ya haki, utawala  wa sheria, utawala bora, Wizara pia imejipanga kutekeleza mkakati wa utoaji wa elimu ya sheria na utawala bora kwa viongozi katika ngazi ya mkoa na wilaya," Amesema DC Mgomi.

Ameongeza kwamba malengo la mkakati huo ni pamoja na kuwajegea uwezo viongozi hao kuhusu haki na wajibu wao kikatiba, kuwaongezea uwelewa katika masuala ya haki za binadamu, uraia, utawala bora  na demokrasia.

Amesema makundi yaliyokusudiwa ni kamati za ulinzi na usalama za mkoa na wilaya, wataalam wa halmashauri na watendaji  wa kata zote za Mkoa wa Songwe.

"Inatarajiwa kuwa utekelezaji wa mkakati huu utawawezesha walengwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki za binadamu,  utawala bora, maadili na miiko ya uongozi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo." Alisema.

Amewaambia wananchi kuwa  madhumuni makuu ya kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia  ni kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na haki za binadamu kwa jamii hususan haki za wanawake na watoto.

Pili, alisema ni kuimarisha huduma ya msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, tatu  kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa sheria kwa umma, masuala ya haki na wajibu  pamoja na misingi ya utawala bora.

"Nne  kutoa elimu ya usimamizi ya mirathi na urirhi, tano utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala hususan  kwa viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji na wajumbe wa mabaraza ya ardhi kwa kushirikiana na wazee maarufu, machifu, viongozi wa dini na viongzi wa Serikali," amesema DC Mgomi.

 Amesema kauli mbiu ya Mama ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inadhihirisha azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulinda, kukuza na kutetea haki za wanawake wanyonge na kupinga ukatili wa kijinsia, kulinda haki za binadamu na kuheshimu utawala wa sheria.

Ameongeza kwamba anaamini kuwa uzingatiaji wa haki za binadamu, utawala bora na utawala wa sheria ni msingi wa maendeleo ya nchi.

"Hakika kampeni hii inatekeleza falsafa ya Rais Samia ya 4R, kwani bila misingi imara  utoaji haki ambayo ni majukumu muhimu ya Wizara ya Sheria na Katiba ni vigumu kutekeleza salsafa hii ya 4R," alisema DC.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Mwandobo, akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya za Mkoa wa Songwe, alisema wana furaha sana na kwa maono ya Rais Samia kupitia kampeni hiyo.

Amesema msaada ywa kisheria wa mama Samia utaenda kutatua kero nyingi ambazo wakuu wa wilaya wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wa kutekeleza majukumu yao.