- Aendesha kituo kuwatibu ‘majeraha’ ya moyo
- Kiongozi, mchechemuzi wa demokrasia
- Aeleza baba yake alivyomjenga kiuongozi
NI mwalimu, mwanaharakati, kiongozi, mshauri, mtafiti, mhamasishaji, anayechanganyika na watu wa rika na kada zote na mwanamke mwenye mchango mkubwa katika maendeleo ya jinsia na demokrasia Tanzania.
Kabla ya kuolewa 1976, alifahamika kwa jina la Mary Mbaga. Lakini baada ya hapo, alianza kuitwa kwa jina la mume.
Akawa Mary Rusimbi ,ambalo mfuatiliaji yeyote wa masuala ya maendeleo na usawa kijinsia nchini, atakuwa analifahamu.
Ni mtoto wa kwanza kwa baba yake, Japhet Omari Mbaga na mama Nandiwe (wote ni marehemu). Hivyo waliokuwa naye kabla ya kuolewa , wanamfahamu kwa jina la Mary Mbaga ambalo anasema kulingana na sera za serikali wakati huo, alilazimika kuitwa kwa jina la ukoo wa mume.
Anasema baada ya kuolewa, utaratibu ulivyokuwa, aliitwa na kuulizwa jina la mume atakalotumia. “Unaleta cheti chako… halafu naanza kuchukua jina la ukoo la mwenzako. Unaanza upya kutumia utambulisho wa mume,” anasema.
Katika mahojiano maalumu na HabariLEO mkoani Dar es Salaam, nabaini Rusimbi ni kinara wa demokrasia, ‘mpishi’wa viongozi wanawake kupitia taasisi na majukwaa mbalimbali aliyoongoza ndani na nje ya nchi.
Ni miongoni mwa wanawake walioshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake uliofanyika Beijing, China mwaka 1995. Pia ni miongoni mwa waanzilishi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) na kuuongoza kwa miaka 10.
Vilevile ni mwanzilishi kisha Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) unaosaidia wanawake ambao aliuongoza kwa miaka 10 kabla ya kustaafu.
Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake Viongozi Afrika kwa upande wa Tanzania (AWLN Tanzania ). Ulizinduliwa Februari, 2020.
Sasa ameanzisha kituo cha ‘kutibu majeraha’ ya moyo ya wanawake kuwapa utulivu wa kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo uongozi wa kisiasa.
ATIBU MAJERAHA YA MOYO
Katika kumjenga mwanamke kiakili, kimtazamo, kisaikolojia na kidemokrasia, Rusimbi anaendesha kituo cha kuwapa wanawake haki ya kupona, kupumzika bila kupingwa, kupata utulivu na amani ya moyo kutokana na makovu yanayosababishwa na mifumo kandamizi ikiwamo mifumo ya kiuongozi.
Kituo hicho ‘Nendiwe Feminist and Coaching Center’ chenye jina la mama yake, anasisitiza kuwa ni msaada kwa wanawake wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa sekta mbalimbali wakiwamo wa kisiasa.
“Hii ni sehemu iliyotengenezwa na wanawake kwa ajili ya wanawake kwa ajili ya ustawi wetu, tuna mikwaruzano mbalimbali maishani , mifumo kandamizi inayotufanya tuwe na makovu,” anasema Rusimbi na kueleza msingi wa kuanzisha kituo hicho baada ya kustaafu WFT.
Anaeleza zaidi, “nimejifunza kwamba sisi kama wanaharakati, hata wanaume hasa vijana wetu, tuna trauma (kukosa utulivu wa moyo), tunakwaruzana, tunafanyiana vituko kuanzia nyumbani, ni machozi, familia kubwa, vinakaa na wewe vinakutafuna.”
“Lakini huna mahali pa kuvitolea. Sasa unatoka nyumbani umeshaudhiwa huko, unatoka na maudhi, unatoka na mikwaruzo, unatoka na hayo mambo ya siku hizi ya umasikini kwenye ngazi ya familia.
“Unatoka na vitu vingi, unaenda ofisini, unamtulia mwenzako hasira. Mwenzako amekuuliza tu kitu kidogo, ni hasira. Tunafanyiana mikwaruzo, tunajeruhiana tunatafuta trauma,” anasema.
Kituo hicho cha Nendiwe, ni maalumu kuwafariji, kuwashauri na kuwatuliza watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wachanga, wanawake waliowahi kufungwa gerezani ili kuwawezesha kupata sehemu salama ya kupata elimu, kubadilishana mawazo na kujikubali kama wanawake.
“Kwa hiyo hiki kituo nilifikiria kukianzisha nilipostaafu iwe ni sehemu ya ya kuturudishia afya ya akili . Mimi si mtaalamu wa afya ya akili lakini ninajiunganisha na wenzangu wa afya ya akili,” anasema.
Katika kituo hicho kilichopambwa na mazingira ya kuvutia, vipo vyumba maalumu vya faragha kwa ajili ya wahitaji wa huduma husika.
Anasema mwanamke akifika hupewa hata nafasi kwa maana ya chumba maalumu cha kulia au hata cha kucheka. “Mlango uko wazi yeyote anakuja. Awe mama wa kijijini, maana wote tunawapatia huduma,” anasema.
Kwa mujibu wa Rusimbi, katika kituo hicho, wanachojaribu ni kuzungumzia afya ya akili.
Akirejelea kazi za kituo hicho, Rusimbi anatamani kuona hata maofisini vituo hivyo vinakuwapo kwa ajili ya ustawi wa moyo na hisia ili kutoa nafasi ya mtu yeyote aliyezidiwa, kupata afya bora ya akili, hisia na kiroho na amani ya moyo.
Anaeleza uzoefu wa watu wanaowahudumia wengi wakiwa wanawake: “…unasikia siku za kwanza mtu anasema mimi sitaki kuongea . Unamwacha kwa sababu hajafika mahala. Lakini mnapoongea, mnapeana moyo, watu wanafunguka stori zao, ndipo mnasikia akisema mimi mwenzenu yamenizidi. Mnaposikia, mnamunganisha na wahusika (wataalamu)”.
Kituoni hapo kuna programu mbalimbali ikiwamo za kujadiliana, kucheka na yoga kwa lengo la kuwekana huru kihisia, kiakili na kisaikolojia hivyo kutokubali kuumizwa na mambo yatokanayo na shughuli mbalimbali ikiwamo za kiuongozi.
Anasema afya ya akili ni ajenda nzito na ya kimaendeleo. “Tumekuwa tunachanganyikiwa halafu tunasema ni maadili. Hili ni tatizo kubwa zaidi ya maadili. Sote tunatakiwa tulifanyie kazi…Na hapa hatuchagui wanawake wa vyama tu bali ni wanawake wote.”
Anakiri kupata ushirikiano wa kutosha wa watu wengi wakiwa wanawake wanaokwenda ‘kupona’ kupitia programu mbalimbali zinazotolewa kituoni hapo.
Kila Jumamosi wana programu ya kutafakari, yoga pamoja na huduma ya afya ya akili. Anasema wametafuta fungu kidogo kwa wasiojiweza kulipa.
Gharama kwa kila programu ya Jumamosi ni Sh 15,000. “Tukimaliza hapo, tunaunda mtandao kwa ajili ya simulizi ambazo zinabomoa vitu vingi sana,” anasema.
Aidha, kituo hicho kimekuwa sehemu ya kukutanisha wanawake kuongea, kucheka , kufurahi na kuondokana na kutingwa kupita kiasi.
“Hata tuliostaafu, naona imekuwa sehemu ya wazee, wanaletwa na watoto wao hasa Jumamosi… Nimeona watoto wanaleta wazazi wao,” anasema.
WATU WALIOMJENGA
Rusimbi anajitathmini kiuongozi akisema baba yake ndiye alimjenga kuanzia ngazi ya familia. Mama yake alijikita kumfanya awe mwanamke mzuri kwenye jamii.
Bibi yake, Namcheja ambaye aliishi naye darasa la kwanza hadi la nne kijijini Usangi, Mwanga anasema alikuwa mwenye bidii, akishiriki masuala ya jamii na aliyejali mapumziko baada ya kazi.
Mwalimu wake wa sekondari ya Zanaki, Tatu Nuru (marehemu) aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan pia anatajwa kumjenga kitaaluma.
Anasema wakati huo, kulikuwa na ubaguzi kati ya weusi na wenye asili ya Asia hivyo Mwalimu Tatu (akiitwa Mrs Mandala), alimpa hamasa. “Alipoona una unafuu wa akili, unaitwa kwake mara kwa mara, alitupa moyo, akisema Waswahili tusitie aibu maana waliokuwa wakifaulu kwenda kidato cha nne walikuwa ni Wahindi,” anasema.
Mwingine ambaye ni chachu katika uongozi na harakati za maendeleo kijinsia, ni mwanasiasa mkongwe, Getrude Mongella. “Hata sasa anakuja hapa kwenye kituo (cha Nendiwe), anaongea na vijana. Tuna ushirikiano naye mpaka leo, namheshimu.”
Vilevile anasema wapo wanawake wengi mfano wa kuigwa akijivunia kuwa nao katika maisha. Anajivunia pia baadhi ya wanaume wakiwamo vijana waliobomoa mfumo kandamizi kwa mwanamke.
RUSIMBI NI NANI?
Alizaliwa mwaka 1953. Anaishi Mbweni, Dar es Salaam, ni mama wa watoto watatu (mmoja alifariki), bibi wa wajukuu watano.
Anapendelea kusoma na kuandika japo anasema: “Tatizo sijajiandika kitabu, naona kama ni aibu kujiandika .Ila nafikiri siku moja nitakaa na kuandika historia yangu.”
Ni mpenzi wa ngoma na dansi licha ya kile anachosema, “Na utu uzima huu…Nahisi ni hobby (upendeleo) ambayo inanitoa kwenye tatizo la afya ya akili…,” anasema akirejelea wimbo wa ‘Bora Nii-enjoy’ wa Bu Jux aliomshirikisha Diamond Platnum unaohimiza kujipa raha.
Huyu ndiye Mary Rusimbi ambaye ameshiriki ipasavyo maendeleo ya mwanamke, aliyeacha ajira ‘nono’ ubalozini kwenda kuongoza harakati hizo kwa vitendo, aliyeandika ‘alama’ nchini katika harakati za jinsia na demokrasia kama itakavyoelezwa katika makala zijazo.