VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA HAVIKUBALIKI
Songwe

Na Mwandishi wetu, Songwe


Mkuu wa Wilaya ya Ileje DC Farida Mgomi, amewaasa wananchi wa Wilaya ya Ileje kuungana, na kushirikiana kwa pamoja kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, kwa kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili ili kuhakikisha jamii inabaki kuwa salama dhidi ya vitendo hivyo.


DC Mgomi ameyasema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia wilayani Ileje.


DC Mgomi ametoa wito kwa wananchi kubadilika na kuachana na vitendo vya ukatili kwani vinarudisha nyuma ustawi wa jamii na kuzorotesha uchumi wa Taifa kwa ujumla. 


Aidha amewasihi wazazi kuwalinda watoto kwa kuwapa malezi stahiki yanayozingatia maadili ya kitanzania ili kuwaepusha watoto kuiga tamaduni za nje ambazo zinakiuka miiko ya maadili ya nchi yetu.


Katika hatua nyingine DC Mgomi ametoa wito kwa familia kudumisha upendo na kuepuka migogoro sambamba na kutumia fursa zilizopo katika Wilaya ya Ileje ili kujiongezea kipato kitakachowasaidia kutunza na kulea familia. 


Mhe. Mgomi ametoa rai kwa Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kuendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaokutwa na hatia ya kujihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mwisho.