Taasisi isiyo ya kiserikali ya Women Writers Forum (WRIFOM), inajishughulisha na uhamasishaji wa usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya habari, na kupaza sauti za wanawake kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo kwenye masuala ya kidemokrasia. WRIFOM inaamini kuwa demokrasia haiwezi kuwa timilifu iwapo ushiriki wa wanawake katika mchakato wa kidemokrasia, utakuwa hafifu.

WRIFOM inakaribisha mawazo ya habari (pitches) kutoka kwa waandishi wa habari Tanzania wanaoweza kuandika habari za wanawake na demokrasia. Ruzuku itatolewa kwa waandishi wanaofanya kazi kwenye magazeti,televisheni, redio na vyombo vya habari mtandao.

Mradi huu unaoanza wakati  Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, umejikita katika kuwatambua wanawake waliochangia kwa kiasi kikubwa kwenye uongozi wa kisiasa na harakati za kudumisha demokrasia nchini.

Ruzuku hii itamwezesha mwandishi kukusanya habari iliyofanyiwa utafiti wa kina, yenye ubunifu na itakayokuwa na matokeo yenye tija kwenye harakati za kuongeza ushiriki wa wanawake katika demokrasia.

Habari inaweza kuwa makala maalum, kipindi maalum cha Redio au Televisheni au makala ya mtandaoni ikimwelezea mwanamke aliyetoa mchango mkubwa kwenye harakati za kidemokrasia nchini.

Wanawake watakaotambuliwa na taarifa zao kuandikwa ni wale waliofanya kazi yenye mchango mkubwa na iliyoacha alama, au walioonyesha uongozi thabiti katika kukabiliana na mfumo dume katika siasa na ambao jitihasa zao zilisaidia katika kubadili mitazamo hasi dhidi ya wanawake katika siasa.

Tunaamini kwa kupaza sauti za wanawake hao, tutaonyesha mafanikio,uwezo wa wao kiuongozi, hali itakayosaidia kuhamasiaha na kuwaongezea kujiamini wanawake wengine wanaposimama kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa.

Sifa za Mwombaji
Mwombaji awe mwandishi wa habari mwanamke anayeshi na kufanyakazi Tanzania Bara. Anaweza kuwa anafanya kazi kwenye magazeti, televisheni na redio au vyombo vya mtandaoni. Maombi kwa waandishi wa habari wa kujitegemea yanahimizwa.

 

Maombi yawe kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili.

Habari ijikite kwenye maeneo haya.

Wazo la Habari
Wazo la habari linapaswa kujikita kwa wanasiasa wanawake, wanaharakati au wengine ambao kazi zao zimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kidemokrasia nchini, lakini habari zao hazijaelezwa kwa kina.

Nani wa kuandikwa?
Wanawake wanasiasa, wanaharakati na wanawake waragibishi wa haki za binadamu na uongozi, ambao wamesimamia kubadili mtazamo hasi kuhusu wanawake walio kwenye siasa,kushawishi mabadiliko na kuhamasisha demokrasia.Wazo la habari lijikite kwa wanawake wa vijijini na maeneo ya kando.

Manufaa
Waandishi watakaoshinda ruzuku hii watapata mafunzo na usaidizi kutoka kwa wabobezi wa tasnia ya habari kwenye kuandika habari za siasa na jinsia. Kila mwandishi atakayechaguliwa atapokea ruzuku ya Dola za Kimarekani 1,000.

Usambazaji wa habari
Habari zitakazokusanywa lazima zichapishwe kwenye vyombo vya habari, pia zitachapishwa kwenye tovuti ya WRIFOM.

 

Uwasilishaji wazo la habari

Uwasilishaji wa wazo la habari kwenye mradi huu utumwe kupitia: https://docs.google.com/forms/d/e/1FAIpQLSeW1NqeQ43rzNYWF0QnRj8IhoSsR96gvcZx93i0H3S1kDnGKg/viewform?vc=0&c=0&w=1&flr=0

Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ni  Agosti 25, 2024