By Elizabeth Zaya
JUMATANO iliyopita ilikuwa na simulizi ya chungu na tamu ya safari ya ukombozi wa mtoto wa kike wa Kimaasai, ndani ya magumu ya utamaduni wao, haki na fursa za kukubalika katika jamii yake ni mtihani mgumu. Endelea na simulizi ya ukaguzi wa mwandishi…
ROSE Njiro (40), anaisimulia Nipashe kuwa pamoja na kupambana kuvunja mila hiyo kandamizi kwa wanawake katika jamii hiyo ya Kimaasai, nguvu nyingine aliitumia kuimarisha kuhakikisha watoto wa kike wanapelekwa shule.
Anasema kwenye jamii hiyo ya Kimaasai, watoto wa kike walikuwa hawaruhusiwi kwenda shule, lakini alipambana kushawishi kuhakikisha wanaandikishwa na kwenda kusoma.
“Zamani ilikuwa kwamba, mwezi wa kwanza wakati watoto kuandikishwa shule, kilikuwa kinakaa kikao cha kijiji, ili waamue mtoto gani apelekwe na hapo wa kike hahesabiki kwenda shule. Kwa hiyo niliamua kuanzisha chekechea katika Kata ya Loliondo (Arusha) na nilienda kwa ujanja ili niwapate watoto wa kike.
“Niliwaambia wazee wa mila kwamba, nataka nijenge Shule ya Kiingereza na nikawaambia kwamba baba yeyote wa familia atakayekubali kuniletea wasichana wawili au watatu kwenye shule ya chekechea, nitamsaidia kusomesha mtoto wa kiume mmoja bure.
“Kwa hiyo walianza kuleta watoto wa kike na nikapata wengi, lakini wakati huo kule shule za serikali hawapeleki watoto, hawaamini katika elimu, bali wanaamini kwamba mifugo ndio kila kitu.
“Ilibidi hadi Ofisa Elimu baada ya kusikia nimepata watoto wengi wa kike waliojiandikisha kuja shule, aje aniulize nimetumia mbinu gani kuwapata hao watoto maana kule kwao hawapelekwi.
“Lengo la kutumia njia hiyo, ndio ilikuwa ujanja wangu ili wakitoka hapo waende darasa la kwanza na waanze kusoma moja kwa moja. Kwa kweli mbinu hiyo ilifanikiwa na baadaye, ile shule niliyojenga ndio ilisababisha kujengwa shule nyingine nyingi za awali Loliondo na Wilaya ya Ngorongoro.
“Nikawa nawaambia, faida za mtoto wa kike na tangu pale wakaanza kuwaruhusu watoto wa kike kwenda shule na mpaka sasa wanaofika hadi vyuo vikuu. Zamani hata watoto wa kiume wenyewe waliokuwa wakipekwa shuleni ilikuwa ni kama adhabu kwao, yaani aliyekuwa akipelekwa shuleni ni mtoto wa mwanamke ambaye hapendwi na mume wake.
“Kwa hiyo, alikuwa akipelekwa kusoma ni kama kumkomoa, kwa sababu walikuwa wanaamini yule anayeachwa kufuga ndio mwenye thamani zaidi,” anasimulia.
UMASAINI LEO
Rose anaeleza kwamba, mpaka sasa watoto wa kike waliopita kwenye mikono yake kwa kuwasimamia kidete wapate elimu ambao wengine wako vyuo vya kati na vyuo vikuu jumla yao 124.
Rose ana maelezo kwamba, kulivyo sasa baada yeye kutoa elimu hiyo, hali imebadilika, jamii imeanza kuamini katika mawazo ya wanawake yameanza kusimama kwenye vikao vya vijiji na hata katika mikutano ya hadhara.
Anafafanua, mawazo yao sasa yanaheshimika zaidi, kuliko ya wanaume, kwa sababu wao wanaposimama wanazungumza ukweli wa yale wanayopinga.
Kwa mujibu wa Rose, mara nyingi wao kinamama ndio wanakuwa wanabaki na familia hasa wanaume wanaposafiri, kwenda kulisha mifugo.
“Kwa mfano kwenye migogoro ya ardhi ikiwamo Pori Tengefu la Loliondo na migogoro mingine mingi, wanawake ndio wamekuwa wakisimama na kutetea hoja kwa sababu sasa hivi wao ndio wanaonekana wamejaliwa hekima namna ya kuwasilisha na siyo wana laana tena.
“Sasa hivi wanaonekana wamejaliwa lugha ya unyenyekevu, kwa hiyo inapokuja masuala magumu kama hayo, kwa sasa wanawatanguliza mbele wanawake ndio wazungumze.
“Kwa hiyo, kwa sasa wanaume wameanza kurudi kwangu, wananipongeza na kunipa majina mazuri wakati hao hao ndio walikuwa wananirushia mawe na kunibatiza majina mabaya,” anasimulia Rose.
VIONGOZI WA KIKE
Rose anasema baada ya kuona elimu aliyowapatia imeanza kueleweka, alianza kupenyeza ajenda ya nyingine ya kupata viongozi wa kike kimila, akiwaona kwa wazee wa mila.
“Mabadiliko hayo yaliyoanza kuonekana, yalinisaidia kunipa nafasi ya kuingia kwenye vikao vya viongozi hao wa mila (Malaigwanani), nikaanza kufanya nao mikutano, kuwahamasisha wamwamini mwanamke.
“Kwa sababu sisi wote tumezaliwa na wazazi, kwa hiyo maumbile yetu yasitufanye sisi hatufai, nikawaambia kwamba hata vitabu vitukufu vya Mungu havitaki ubaguzi, nikaendelea kuwahamasisha ili kuvunja ile mitazamo yao hasi kwa mwanamke.
“Ilinichukua muda mrefu mpaka kuwaaminisha na kuwashawishi wamwamini mwanamke na kumpa nafasi kwa sababu si rahisi kitu ambacho wameamini katika maisha yao, kiwatoke mara moja.
“Nilienda nao taratibu hivyo hivyo, wanakwenda wanaamini wachache, hivyo hivyo naendelea kuwashika, na nikawa nawakutanisha viongozi hao wa mila na vyombo vya dola, Jeshi la Polisi, TAKUKURU, wakuu wa idara wa halmashauri, ustawi wa jamii.
“Baadhi ya wanawake ambao ni viongozi katika nyanja mbalimbali serikalini na kwenye taasisi, nawachanganya humo” anaeleza Rose, akinena lengo la kufanya hivyo, ni kuiteka jamii yake ielewe watu wote ni muhimu na wanategemeana.
“Nilikuwa nawakutanisha na wanawake viongozi kutoka katika nyanja tofauti, ili wajifunze na waone kwamba mbona hawa ni wanawake na wanaongoza, kwanini isiwe katika jamii yetu, nikitaka waone kwamba sisi sote ni viungo vinavyotegemeana.
VIONGOZI WA KIKE
“Baada ya kuona kwamba wameanza kunielewa, ikabidi nianze kuwadadisi kwamba kwa nini huwa hakuna viongozi wanawake wa mila. Nikaanza tena kuwaelimisha na kwa sababu tayari wameanza kuelewa kwamba mwanamke ana uwezo.
“Ikabidi na wao wakae wazungumze na wakaja na tamko mwaka jana 2023 kwamba, wamebariki kuwapo na viongozi wa kike kwenye jopo la viongozi wa kimila.
“Mwaka huu Julai tukawasimika wanawake sita (Mangaigwanani) kuingia kwenye jopo hilo la viongozi wa kiume wa kimila (Malaigwanani) na kulikuwa na sherehe kubwa kusherehekea jambo hili kubwa la kihistoria ambalo halijawahi kutokea tangu jamii hii iundwe.
“Na sherehe ziligharimiwa na viongozi wa kiume wenyewe wa kimila na ndio walitangaza rasmi kwamba sasa mwanamke anaruhusiwa kuwa kiongozi na atakuwa na uwezo wa kusimama mahali popote kwenye nyanja ya uongozi iwe wa kimila au serikali.
“Katika sherehe hizi za kuwasimika wanawake viongozi wa kimila, viongozi wa serikali nao walialikwa. llikuwa ni gumzo na mshangao mkubwa kwa jamii ya kimaasai kumkubali mwanamke lakini ndio ikawa imekuwa.
“Kwa hiyo, kwa sasa tuna wanawake viongozi kutoka ata sita za wilaya ya Ngorongoro ni mapinduzi ya kihistoria yamefanyika,” anasema Rose.
Anafafanua kuwa, kwa sasa wanawake ndio wanaowatumia kuwahamasisha kinamama wenzao kusimama kwenye nafasi za uongozi kwa kuanzia katika uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa.
Hapo anarejea kwamba, hadi sasa wana orodha kubwa mpaka ya wanawake waliojiandikisha kugombea katika nafasi ya uchaguzi ujao wa serikali za mitaa mwaka huu.
HAKI YA KURA
Rose anasema zamani mwanamke wa jamii ya kimaasai alikuwa hana uamuzi na kura yake, alikuwa analazimishwa achague yule ambaye mume wake anataka na kura haikuwa siri kwa upande wake.
Lakini sasa, nalo wamewaelimisha na wameacha kuwalazimisha kuchagua watu wasiowataka. Anafafanua:
“Zamani mwanamke wa Kimaasai huna uamuzi na kura yako, sehemu ambayo mume wako anapita, ndio hapohapo na wewe unatakiwa upite, hata kama hutaki, na ilikuwa hakuna siri unaambiwa utamke kwa sauti ili wasikie je umeenda tofauti na mume wako?
“Lakini sasa, wamejua haki zao, sasa hivi wanawake wanasema kura ni siri, hutakiwi kupiga kwa sauti na unamchagua unayemtaka siyo kuchaguliwa na mtu, kwa hiyo sasa hivi wamejua kura ni haki yao.”