UPANDIKIZAJI WA NYONGA BANDIA TANZANIA.
Dar es Salaam

http://upandikizaji//nyonga//bandia//yzu/daressalaam//tanzania

By Naomi Achieng

Ni nadra kusikia mtu akisumbuliwa na ugonjwa wa nyonga, hata hivyo maradhi hayo sasa yamekuwa ya kawaida hasa kwa watu wenye umri wa miaka 50 au zaidi huku wengine walio chini ya umri huo wakiyapata kutokana na visababishi tofauti. 

Matibabu ya ugonjwa huo yalianza kutolewa katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) mwaka 2014 ambapo uwekezaji mkubwa wa wataalamu wa matibabu hayo pamoja na vifaa vya kisasa, ulianza kufanyika. 

MOI inakiri kwamba kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa nyonga tangu walipoanza kutoa huduma hiyo hapa nchini.

Hadi sasa, MOI imefanya mapinduzi makubwa kwenye matibabu hayo kwa kuwa huduma hiyo inatolewa hapa nchini kwa ukamilifu wake na kuwasaidia Watanzania kuepukana na gharama za ziada endapo angefuata matibabu hayo nje ya nchi. 

Daktari bingwa wa mifupa aliyebobea katika upandikizaji wa nyonga bandia kutoka MOI, Karama Kenyunko, anasema tatizo la nyonga ni kubwa kwa kuwa watu wenye umri mkubwa nyonga zao zinaharibika. 

Kwa kuzingaia hilo, Dk Kenyunko anasema taasisi hiyo inahakikisha kwamba nyonga bandia zinapatikana hapa nchini. Anasema kabla ya mwaka 2014, wagonjwa walikuwa wanakwenda nje ya nchi kupata matibabu hayo lakini kwa sasa matibabtu ya nyonga bandia yanapatikana hapa nchini. 

“Idadi ya waathirika kati ya wanaume na wanawake ni sawa, haitofautiani kwa sababu kisababishi kikubwa ni umri, kwa hiyo idadi haitofautiani sana kati ya wanawake na wanaume,” anasema daktari. 

Daktari huyo bingwa anasema operesheni ya kuweka nyonga bandia inatumia saa moja na kama tatizo ni kubwa zaidi, wanatumia saa moja na nusu. Anasema hilo linawezeshwa na kuwepo kwa ujuzi na uwekezaji wa vifaa vya kisasa katika taasisi hiyo. 

“Ili operesheni hii ifanyike, mgonjwa anafanyiwa vipimo mbalimbali kwa ujumla ili kuona kama anaweza kufanyiwa upasuaji. Anaangaliwa na madaktari bingwa zaidi ya watatu, ataonwa na daktari bingwa wa upandikizaji mifupa, ataonwa na daktari bingwa wa dawa za usingizi, ataonwa na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, ataonwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo. Hiyo yote ni kuhakikisha operesheni yetu inakuwa na mafanikio makubwa,” anasema. 

Wanaofanyiwa upasuaji huo daktari huyo anasema operesheni ya upandikizaji wa nyonga bandia hufanyika kwa mtu mwenye uhitaji ambaye nyonga zake zimesagika  au  hawezi kuitumia kwa sababu inamsababishia maumivu makali, kwa hiyo inabidi kubadilisha ili aendelee na maisha yake kama kawaida. 

Dk Kenyunko anasema vitu ambavyo vinaweza kuharibu nyonga ni pamoja na umri mkubwa, ajali, wagonjwa wa seli mundu na watu ambao wanazaliwa nyonga zao zikiwa hazijajijenga vizuri na wangonjwa wanaotumia steroid kwa wingi. 

“Nyonga ni moja ya kiungo ambacho kinabeba uzito mkubwa ndani ya mwili, kwa hiyo kadiri unavyokuwa mtu mzima nazo zinazeeka, kwa hiyo inabidi kubadilisha,” anasema daktari huyo bingwa wa nyonga. 

Akifafanua kuhusu steroids, anasema ni dawa ambazo zikitumika kwa muda mrefu zinasababisha nyonga kuharibika. 

“Asilimia kubwa ya watu tunaowabadilisha nyonga ni wale watu wazima kuanzia miaka 50 na kuendelea. Hao wanaokuwa chini ya huo umri, wanakuwa na visababishi mbalimbali kama nilivyovitaja awali,” anaeleza Dk Kenyunko.

 Hata hivyo, anaonya kwamba nyonga anazowekewa mgonjwa haina maana kwamba atakaa nazo maisha yake yote, bali zina muda wake, wanatarajia akae nayo kwa miaka 10, 15 au 20.

 Mmoja wa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa nyonga katika Taasisi ya MOI, Ally Mohamed Mwinyi, mkazi wa Zanzibar, anasema amesumbuliwa na nyonga kwa muda wa mwaka mmoja sasa. Hata hivyo, anaeleza kwamba tatizo hilo lilianza alipokuwa na umri wa miaka 15 baada ya kuumia wakati akicheza mpira na wenzake. 

"Nilipokuwa nimeumia, nilikwenda Hospitali ya Mnazi Mmoja (iliyopo Zanzibar) nikapata nafuu). Tatizo limekuja kuanza tena nilipofikia umri wa utu uzima," anasema Mwinyi. Anasema baada ya kufanyiwa upasuaji MOI, sasa amepata nafuu kwani alikuwa hawezi kusogeza hata kiti kilichopo jirani yake, lakini sasa anaweza kufanya hivyo”.

Utaratibu huu unafanyika hapa jijini Dar es Salaam ambapo inaripotiwa kuwa huduma hiyo ilitolewa kwa mara ya kwanza nchini mwaka 2004 katika Taasisi ya Mifupa (MOI). Sasa hata baadhi ya hospitali binafsi za Dar es Salaam zinafanya shughuli hizo. 

Upasuaji wa kubadilisha nyonga ni utaratibu ambao daktari hubadilisha nyonga kwa kuweka kiungo bandia ambacho mara nyingi hutengenezwa kutokana na chuma na plastiki. Upasuaji kama huo wa uingizwaji wa nyonga bandia unapaswa kufanyika kama chaguzi zingine za matibabu zimeshindwa kupunguza maumivu ya viungo. 

Maumivu ya viungo hayavumiliki, hivyo madaktari wanalazimika kuibadilisha na ile ya bandia. Madaktari wanaweza kuiita kama nyonga bandia. Utaratibu ni salama lakini unachukua muda mrefu, kama saa 3 hadi 6 kutegemeana na daktari wa upasuaji na masuala katika eneo husika. 

Daktari wa upasuaji atakata kiasi kando ya nyonga na kusogeza misuli iliyounganishwa na sehemu ya juu ya mfupa wa paja ili kuweka wazi kifundo cha nyonga. Kisha sehemu ya kifundo ya inasogezwa vizuri kwa kukata mfupa wa paja kwa msumeno uliotengenezwa kwa ajili ya upasuaji, kisha kiungo bandia kilichotayarishwa kinaunganishwa kwa uangalifu kwenye mfupa wa paja kwa kutumia simenti au nyenzo zinazoruhusu mfupa uliobaki kuunganishwa kwenye kiungo kipya.

Mwisho.