Na Mwandishi Wetu
Songwe
MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi ametoa wito kwa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kushiriki kikamilifu katika suala zima la utunzaji wa amani hasa kipindi hiki ambacho Nchi inaelekea katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
DC Mgomi ameyasema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya Jeshi la Akiba Wilayani Ileje katika Kata ya Isongole ambapo amewahimiza wahitimu hao kushiriki katika suala zima la ulinzi wakati wa uchaguzi Novemba 27, 2024.
"Tunatarajia kuona mnayatumia vizuri mafunzo haya, na Serikali ya Wilaya inawaamini na kuwategemea sana katika kulinda amani na usalama wa Nchi," amesema.
Aidha Mgomi amesisitiza juu ya umuhimu wa kutumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko chanya katika jamii ikiwemo suala zima la kuwa macho ya Serikali katika kuibua maovu katika jamii lakini pia kutekeleza majukumu wanayopewa na viongozi wao pasina kujali hali.
"Nyinyi sasa ndo mtakuwa macho na masikio kwa serikali kwa kutoa taarifa ya viashiria vibaya vya Nchi...msiwe watu wa kufata mkumbo na badala yake muwe wazalendo watiifu, hodari na waadilifu," amesema.
Pia, Mgomi amewahakikishia wahitimu hao kuwa Serikali inatambua changamoto zilizopo hususani wakati wa mafunzo hivyo kupitia Ofisi yake changamoto zimepokelewa kama zilivyoainishwa katika risala na kuahidi kufanyiwa kazi ili kuendelea kutambua nafasi ya Jeshi la Akiba katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Jumla ya wahitimu 174 wamehitimu mafunzo hayo huku wanaume wakiwa 148 na Wanawake 26.
Mwisho