MASHABIKI WA KANDANDA TANZANIA MAMBO MAZURI
Dar es Salaam

Na Naomi Achieng'

Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewalipia viingilio Watanzania wote kwenda uwanjani na kushuhudia mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Guinea katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo unachezwa leo Novemba 19, 2024 ambapo Taifa Stars itakuwa nyumbani kumenyana  na Guinea katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2025) nchini Morocco.

Taarifa hii imetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ambapo amesema Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa watu wote waingie uwanjani bure na hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwenda kuipa hamasa Taifa Stars ili ifanikiwe kusonga mbele katika michuano hiyo.

Taifa Stars inahitaji ushindi tu ili kujihakikishia tiketi ya kushiriki Afcon mwakani nchini Morocco.

Msimamo wa kundi H, hivi sasa DR Congo ndio kinara ikiwa na pointi 12 ikifuatiwa na Guinea yenye 9, Stars ikishika nafasi ya tatu na pointi 7 huku Ethiopia akiburuza mkia na pointi 1.

Mwisho.